Uhakiki wa ubunilizi wa changamoto za ndoa katika riwaya teule za kiswahili kiuhusika na kiusimulizi
Abstract/ Overview
Ndoa ni asasi muhimu inayoiendeleza jamii na kudumisha uthabiti wake kupitia majukumu yake muhimu ya kuhakikisha wanajamii wapya wanazaliwa na kulelewa. Tafiti za kifasihi na za kisosholojia kuhusu ndoa zinaonyesha kuwa inaendelea kukosa uthabiti na kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Tafiti za awali kuhusu ndoa katika fasihi ya Kiswahili zimebainisha changamoto zinazoiyumbisha na kufanya ishindwe kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Hata hivyo, tafiti hizi zimeegemea uchunguzi wa usawiri wa maudhui ya ndoa katika kazi mahususi za kifasihi.Kuna haja ya kuchunguza namna changamoto za ndoa zimejengwa kupitia vipengele vya kibunilizi kwa kurejelea kazi mbalimbali za kifasihi. Kwa msingi huu, utafiti huu unahakiki namna uhusika na usimulizi umetumika kujenga changamoto za ndoa katika riwaya tofauti za Kiswahili zilizoandikwa na waandishi tofauti. Lengo la utafiti huu ni kuhakiki uhusika na usimulizi katika ubunilizi wa changamoto za ndoa katika riwaya teule za Kiswahili. Madhumuni ya utafiti huu ni; kueleza jinsi changamoto za ndoa zimesawiriwa kupitia usawiri wa wahusika katika riwaya teule za Kiswahili; kutathmini namna athari za changamoto za ndoa zimedhihirishwa kupitia usawiri wa wahusika katika riwaya teule za Kiswahili na hatimaye kufafanua namna njia za kukabiliana na changamoto za ndoa katika riwaya teule za Kiswahili zimewasilishwa kupitia mbinu za usimulizi. Utafiti huu unaongozwa na mseto wa nadharia ya umuundo- uamilifu kwa mujibu wa Merton (1957) na nadharia ya naratolojia kwa mujibu wa Genette (1980) na Kenan (1983). Muundo wa utafiti huu ni wa kiuchanganuzi. Eneo la utafiti huu ni la maktaba, muktadha wa fasihi na mahususi riwaya ya Kiswahili. Kundi lengwa ni riwaya za Kiswahili ambazo zimesawiri changamoto za ndoa. Usampulishaji dhamirifu uliwezesha kubainishwa kwa sampuli ya riwaya tano zifuatazo; Kiu (1972), Mwisho wa Kosa (1987), Maisha Kitendawili (2000), Ua la Faraja (2005) na Unaitwa Nani? (2008). Data ilikusanywa kutoka kwa riwaya teule kwa kutumia mbinu ya unukuzi kwa kutumia orodha ya uchunzaji. Data ilichanganuliwa kimaudhui na kuwasilishwa kimaelezo. Matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kwamba changamoto za ndoa kama vile umaskini zimesawiriwa kupitia uhusika wao kimatendo, kiusemi, kimazingira na wa muonekano wa nje. Aidha yanaonyesha kuwa athari za changamoto za ndoa kama vile ukosefu au upungufu wa mahitaji ya kimsingi zimedhihirishwa na wahusika kupitia uhusika wao kimatendo, kiusemi, kimazingira na kwa muonekano wa nje. Hatimaye, matokeo haya yanaonyesha kuwa njia za kukabilia na changamoto za ndoa kama vile ushauri nasaha zimewasilishwa kupitia mbinu zifuatazo za usimulizi; usimulizi wa nafsi ya kwanza, usimulizi wa nafsi ya tatu, mtazamo wa ndani, mtazamo wa nje, msimulizi tawasifu, msimulizi wasifu na msimulizi horomo. Matokeo yanaonyesha tofauti na kulingana katika matumizi ya uhusika na usimulizi katika kujenga changamoto za ndoa kwenye riwaya teule. Utafiti huu unatarajiwa kuonyesha namna uumbaji wa wahusika na mbinu za usimulizi zinasawiri maudhui; unachangia utafiti zaidi kuhusu ndoa katika fasihi ya Kiswahili kwa kuhakiki ubunilizi wa changamoto zake na kupanua uelewa kuhusu changamoto hizi.